Mabingwa mara sita wa soka barani Afrika Al Ahly ya Misri wamefufua matumaini ya kufika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Ubingwa wa Afrika baada ya kutoka sare ya goli 1-1 na Wydad Casablanca, katika mchezo wa robo fainali uliochezwa leo kule nchini Morrocco.
Mshambuliaji wa Misri Mohamed Gedo maarufu kama Nagy alikuwa wa kwanza kufunga bao katika dakika ya 37 kabla ya Abdurahim Benkajane kusawazisha goli hilo zikiwa zimesalia dakika mbili kabla ya mapumziko.
Nayo klabu ya Tunisia ya Esperance imekalia kiti cha uongozi wa kundi B, baada jana kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Molodia Alger ya Algeria.
Kwa matokeo hayo ni Molodia tu wanaweza kufika hatua ya timu nne za mwisho za nusu fainali kutoka kundi B.
Mejdi Traore alikuwa wa kwanza kuifungia mabao Esperance katika dakika ya tisa.
Bao la pili lilipachikwa na Mkameruni Joseph Ndjeng ambaye alifanikiwa baadae kufunga mabao mengine mawili na kuhesabu mabao matatu aliyofunga peke yake.
Katika mechi za mwisho za makundi kati ya tarehe 16-18 mwezi huu wa Septemba, Ahly itakabiliana na Esperanace huku Wydad hawana budi kusafiri hadi Algeria kuikabili Mouloudia.
Klabu ya Enyimba ya Nigeria ilikuwa ya kwanza kufuzu hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Soka barani Afrika walipoilaza Al Hilal ya Sudan mabao 2-1siku ya Ijumaa.
No comments:
Post a Comment