CHAMA cha soka wilaya ya Mbeya mjini (MUFA) kimesema kupatikana kwa ufadhili katika ligi ya taifa ngazi ya wilaya inayotarajia kuanza kutimua vumbi Septemba 17 mwaka huu kutaleta chachu ya ushindani tofauti na misimu iliyopita.
Uongozi wa MUFA umebainisha hayo kufuatia kampuni ya usambazaji kompyuta ya Access Computer Ltd (ACL) ya jijini Mbeya kutangaza kudhamini ligi hiyo inayotarajia kushirikisha jumla ya timu 13.
Mwenyekiti wa Mufa, John Gondwe, amesema kampuni ya ACL itadhamini ligi hiyo kwa kutoa zawadi mbalimbali kwa washindi ambapo mshindi wa kwanza atazawadiwa shilingi laki tatu na seti moja ya jezi na mpira mmoja.
Ameongeza kuwa kwa mshindi wa pili atazawadiwa shilingi laki moja na nusu na seti moja ya jezi na mpira mmoja ,ambapo mshindi wa tatu atazawadiwa shilingi laki moja na seti moja ya jezi na mpira mmoja huku zawadi kwa mchezaji,mlinda mlango ,mwamuzi na kocha bora zikitarajiwa kutangazwa baadaye na kampuni hiyo.
Gondwe amesema lengo la udhamini huo kwa chama na wadau kwa pamoja ni kuona ligi inapata msisimko tofauti na miaka ya nyuma ambapo timu zilizoibuka bingwa ziliishia kukabidhiwa kombe bila zawadi ya aina yoyote.
Kwa mujibu wa Gondwe timu ambazo zimethibitisha kushiriki ligi hiyo ni pamoja na Zaragoza FC,Black Scopion,Airpot Rangers, Eleven na Ilemi Shooting Stars Boys.
Timu zingine ni Winers FC,Super Cargo,African Boys,Ilomba, Town Stars,Uyole Stars, Vijana FC na Iyunga Stars.
No comments:
Post a Comment