Tuesday, September 13, 2011

VAN DER VAAT AILAA TOTTENHAM

                                      
Kiungo mshambuliaji wa Tottenham Rafael van der Vaart amesema amekasirishwa na kitendo cha kuachwa katika kikosi cha timu hiyo kitakachoshiriki Ligi ya Europa.

Van der Vaart alitoka akichechemea wakati Spurs ilipofungwa mabao 5-1 na Manchester City na awali ilielezwa asingeweza kucheza kwa muda wa wiki sita akiuguza msuli wake wa paja.

Lakini licha ya sasa akiwa anatarajiwa kupona na kuweza kucheza mechi dhidi ya Liverpool siku ya Jumapili,ila kuenguliwa kwake kuna maana kwamba mchezaji huyo atakosa mechi sita za makundi za ligi ya Europa.
Hata hivyo amesema hayo anayapa kisogo na anajiandaa kwa pambano dhidi ya Liverpool na ameonesha matumaini atakuwa amepona kabisa hadi wakati huo.

Mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid alikosa kuiwakilisha nchi yake ya Uholanzi kwa mashindano ya kufuzu kwa Euro 2012 na pia hakupangwa katika mechi ya kwanza kwa Spurs kushinda msimu huu dhidi ya Wolves siku ya Jumamosi.

Meneja wa Spurs Harry Redknapp anakusudia kuchezesha damu changa kama Harry Kane, Tom Carroll na Jake Livermore katika Ligi ya Europa ili kukiweka kikosi chake tayari kwa ajili ya patashika za Ligi Kuu ya England.

Spurs wataanza mtanange wa Ligi ya Europa League dhidi ya PAOK Salonika nchini Ugiriki siku ya Alhamisi.

Iwapo watafanikiwa kusonga mbele katika hatua ya makundi, wataruhusiwa kusajili wachezaji wengine watatu wapya.

No comments:

Post a Comment